(12) Ewe Nabii! Watakapo kujia wanawake Waumini wanakuahidi ya kwamba hawatamshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote, wala hawataiba, wala hawatazini, wala hawatawauwa watoto wao, wala hawataleta uzushi wanao uzua tu wenyewe baina ya mikono yao na miguu yao, wala hawatakuasi katika jambo jema, basi peana nao ahadi, na uwatakie maghfira kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi maghfira, Mwenye kurehemu.
(13) Enyi mlio amini! Msiwafanye rafiki zenu watu ambao Mwenyezi Mungu amewakasirikia. Hao wamekwisha kata tamaa ya Akhera, kama makafiri walivyo wakatia tamaa watu wa makaburini.
الصف As-Saff
(1) Vinamtakasa Mwenyezi Mungu viliomo katika mbingu na katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
(2) Enyi mlio amini! Kwa nini mnasema msiyo yatenda?
(3) Yanachukiza vikubwa mno kwa Mwenyezi Mungu kuwa mnasema msiyo yatenda.
(4) Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao pigana katika Njia yake kwa safu kama jengo lilio kamatana.
(5) Na Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Kwa nini mnaniudhi, nanyi mnajua kuwa hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu niliye tumwa kwenu? Walipo potoka, Mwenyezi Mungu aliziachia nyoyo zao zipotoke. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.