(72) Akasema: Je, hivyo mimi nizae, na hali yangu ni kikongwe na huyu mume wangu ni kizee? Hakika haya ni mambo ya ajabu!
(73) Wakasema: Je, unastaajabia amri ya Mwenyezi Mungu? Rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake ziko juu yenu, enyi watu wa nyumba hii! Hakika Yeye ndiye Msifiwa wa kutukuzwa.
(74) Basi khofu ilipo mwondoka Ibrahim, na ikawa ile bishara imemfikia, alianza kujadiliana nasi juu ya kaumu ya Lut'.
(75) Hakika Ibrahim alikuwa mpole, ana huruma, na mwepesi wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu.
(76) (Akaambiwa): Ewe Ibrahim! Wachilia mbali haya! Kwa hakika amri ya Mola wako Mlezi imekwisha kuja, na hakika hao itawafikia adhabu isiyo rudi nyuma.
(77) Na wajumbe wetu walipo kuja kwa Lut' aliwahuzunukia na akawaonea dhiki. Akasema: Hii leo ni siku ngumu!
(78) Wakamjia kaumu yake mbio mbio. Na kabla ya haya walikuwa wakitenda maovu. Yeye akasema: Enyi watu wangu! Hawa binti zangu, ndio wametakasika zaidi kwenu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi mbele ya wageni wangu. Hivyo, hamna hata mtu mmoja miongoni mwenu aliye ongoka?
(79) Wakasema: Bila shaka umekwisha jua hatuna haki juu ya binti zako, na unayajua tunayo yataka.
(80) Akasema: Laiti ningeli kuwa na nguvu kwenu, au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu!
(81) (Wajumbe) wakasema: Ewe Lut'! Sisi ni wajumbe wa Mola wako Mlezi. Hawa hawatakufikia. Na wewe ondoka pamoja na ahali zako usiku ungalipo. Wala yeyote miongoni mwenu asitazame nyuma, isipo kuwa mkeo, kwani yeye utamfika msiba utakao wafika hao. Hakika miadi yao ni asubuhi. Je, asubuhi si karibu?