(92) Na haiwi Muumini kumuuwa Muumini ila kwa kukosea. Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukosea basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe diya kuwapa jamaa za maiti, isipo kuwa waache wenyewe kuwa ni sadaka. Na akiwa ni jamaa wa maadui zenu, hali yeye ni Muumini, basi ni kumkomboa mtumwa aliye Muumini. Na akiwa ni miongoni wa watu ambao pana ahadi baina yenu na wao basi wapewe diya watu wake na akombolewe mtumwa Muumini. Na asiye pata, basi afunge miezi miwili mfululizo, kuwa ni toba kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima.
(93) Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannamu humo atadumu, na Mwenyezi Mungu amemkasirikia, na amemlaani, na amemuandalia adhabu kubwa.
(94) Enyi mlio amini! Mnapo safiri katika Njia ya Mwenyezi Mungu basi hakikisheni, wala msimwambie anaye kutoleeni salamu: Wewe si Muumini; kwa kutaka manufaa ya maisha ya dunia hii, hali ya kuwa kwa Mwenyezi Mungu zipo ghanima nyingi. Hivyo ndivyo mlivyo kuwa nyinyi zamani, na Mwenyezi Mungu akakuneemesheni. Basi chunguzeni sawa sawa. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.