(234) Na wale miongoni mwenu wanao kufa na wakaacha wake, hawa wake wangoje peke yao miezi mine na siku kumi. Na wanapo timiza eda yao basi hapana ubaya kwao kwa wanao jifanyia kwa mujibu wa ada. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote mnayo yatenda.
(235) Wala si vibaya kwenu katika kupeleka posa kwa ishara tu kwa wanawake waliomo edani au mkadhamiria katika nyoyo zenu. Mwenyezi Mungu anajua kwamba nyinyi mtawakumbuka. Lakini msiwaahidi kwa siri, ila mnene maneno mema. Wala msiazimie kufunga ndoa mpaka eda ifike mwisho wake. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo katika nafsi zenu. Basi tahadharini naye. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mpole.
(236) Hapana ubaya kwenu mkiwapa t'alaka wanawake ambao hamjawagusa au kuwabainishia mahari yao. Lakini wapeni cha kuwaliwaza, mwenye wasaa kadiri awezavyo na mwenye dhiki kadiri awezavyo - maliwaza kwa mujibu wa dasturi kuwa ni haki juu ya watendao mema.
(237) Na mkiwapa t'alaka kabla ya kuwagusa, na mmekwisha wawekea hayo mahari makhsusi, basi wapeni nusu ya mahari mlio agana, isipo kuwa ikiwa wanawake wenyewe wamesamehe, au mume ambaye kifungo cha ndoa ki mikononi mwake awe amesamehe. Na kusameheana ndiko kulio karibu zaidi na uchamngu. Wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.