(75) Na lau tungeli warehemu na tukawaondolea shida waliyo nayo bila ya shaka wangeli endelea katika upotofu wao vile vile, wakitangatanga.
(76) Na hakika tuliwatia adhabu kali; lakini hawakuelekea kwa Mola wao Mlezi wala hawakunyenyekea.
(77) Mpaka tulipo wafungulia mlango wa adhabu kali, hapo ndipo wakawa wenye kukata tamaa.
(78) Na Yeye ndiye aliye kuumbieni kusikia na kuona na nyoyo za kufahamu. Ni kuchache mno kushukuru kwenu.
(79) Na Yeye ndiye aliye kuenezeni katika ardhi, na kwake Yeye mtakusanywa.
(80) Na Yeye ndiye anaye huisha na kufisha, na yake Yeye mabadiliko ya usiku na mchana. Basi je! Hamfahamu?
(81) Bali wanasema kama walivyo sema watu wa kwanza.
(82) Walisema: Je! Tukisha kufa tukawa udongo na mifupa ndio tutafufuliwa?
(83) Tuliahidiwa haya sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni visa vya uwongo vya watu wa zamani.
(84) Sema: Ni ya nani ardhi na viliomo ndani yake, kama nyinyi mnajua?
(85) Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu! Sema: Basi, je, hamkumbuki?
(86) Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu saba na Mola Mlezi wa A'rshi Kuu?
(87) Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Sema: Basi je, hamwogopi?
(88) Sema: Ni nani mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu, naye ndiye anaye linda, wala hakilindwi asicho taka, kama mnajua?
(89) Watasema: (Ufalme huo) ni wa Mwenyezi Mungu. Sema: Basi vipi mnadanganyika?