(12) Na fungu lenu ni nusu walicho acha wake zenu ikiwa hawana mtoto. Wakiwa na mtoto basi fungu lenu ni robo ya walicho acha, baada ya wasia waliyo usia au kulipa deni. Na wake zenu watapata robo mlicho kiacha, ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumni ya mlicho kiacha, baada ya wasia mlio usia au kulipa deni. Na ikiwa mwanamume au mwanamke anaye rithiwa hana mtoto wala wazazi, lakini anaye ndugu mume au ndugu mke, basi kila mmoja katika hawa atapata sudusi. Na wakiwa zaidi kuliko hivyo basi watashirikiana katika thuluthi, baada ya wasia ulio usiwa au kulipa deni, pasio kuleta dhara. Huu ndio wasia ulio toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mpole.
(13) Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na anaye mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Yeye atamtia katika Pepo zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.
(14) Na anaye muasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akaipindukia mipaka yake, (Mwenyezi Mungu) atamtia Motoni adumu humo, na atapata adhabu ya kudhalilisha.