(10) Bila ya shaka wanao fungamana nawe, kwa hakika wanafungamana na Mwenyezi Mungu. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao. Basi avunjaye ahadi hizi anavunja kwa kuidhuru nafsi yake; na anaye tekeleza aliyo muahadi Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atamlipa ujira mkubwa.
(11) Watakuambia mabedui walio baki nyuma: Yametushughulisha mali yetu na ahali zetu, basi tuombee msamaha. Wanasema kwa ndimi zao yasiyo kuwamo katika nyoyo zao. Sema: Ni nani awezaye kukusaidieni chochote kwa Mwenyezi Mungu akitaka Yeye kukudhuruni au akitaka kukunufaisheni? Bali Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
(12) Lakini mlidhani kwamba Mtume na Waumini hawatarudi kabisa kwa ahali zao, na mkapambiwa hayo katika nyoyo zenu, na mkadhania dhana mbaya, na mkawa watu wanao angamia.
(13) Na asiye muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi kwa hakika Sisi tumewaandalia makafiri Moto mkali.
(14) Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Humsamehe amtakaye, na humuadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(15) Walio baki nyuma watasema: Mtapo kwenda kuchukua ngawira, tuacheni tukufuateni! Wanataka kuyabadili maneno ya Mwenyezi Mungu. Sema: Hamtatufuata kabisa. Mwenyezi Mungu alikwisha sema kama hivi zamani. Hapo watasema: Bali nyinyi mnatuhusudu. Siyo, bali walikuwa hawafahamu ila kidogo.