(87) Wameridhia kuwa pamoja na wabakiao nyuma, na nyoyo zao zikapigwa muhuri; kwa hivyo hawafahamu.
(88) Lakini Mtume na wale walio amini pamoja naye waliwania Jihadi kwa mali zao na nafsi zao. Hao ndio watakao pata kheri nyingi, na hao ndio wenye kufanikiwa.
(89) Mwenyezi Mungu amewatengenezea Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
(90) Na walikuja wenye kutoa udhuru katika Mabedui ili wapewe ruhusa, na wakakaa wale walio mwambia Mwenyezi Mungu na Mtume wake uwongo. Itawafika walio kufuru katika wao adhabu chungu.
(91) Hapana lawama kwa wanyonge, wagonjwa, na wasio pata cha kutumia, maadamu wanamsafia niya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hapana njia ya kuwalaumu wanao fanya wema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
(92) Wala wale walio kujia ili uwachukue ukasema: Sina kipando cha kukuchukueni. Tena wakarudi na macho yao yanamiminika machozi kwa huzuni ya kukosa cha kutoa.
(93) Ipo njia ya kuwalaumu wale wanao kuomba ruhusa wasende vitani na hali wao ni matajiri. Wameridhia kuwa pamoja na wanao bakia nyuma. Na Mwenyezi Mungu amewapiga muhuri juu ya nyoyo zao. Kwa hivyo hawajui.