(21) Na tunapo waonjesha watu rehema baada ya shida waliyo ipata, utawaona wana vitimbi kuzipangia Ishara zetu. Sema: Mwenyezi Mungu ni Mwepesi zaidi wa kupanga. Hakika wajumbe wetu wanayaandika mnayo yapanga.
(22) Yeye ndiye anaye kuendesheni bara na baharini. Hata mnapo kuwa majahazini na yakawa yanakwenda nao kwa upepo mzuri wakaufurahia, upepo mkali ukawazukia, na yakawajia mawimbi kutoka kila upande, na wakaona wamesha zongwa, basi hapo humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafishia niya: Ukituokoa na haya bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa wanao shukuru.
(23) Lakini akisha waokoa, mara wanafanya jeuri tena katika nchi bila ya haki. Enyi watu! Jeuri zenu zitakudhuruni wenyewe. Hii ni starehe ya maisha ya dunia tu. Kisha marejeo yenu ni kwetu, na hapo tutakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
(24) Hakika mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tuliyo yateremsha kutoka mbinguni, kisha yakachanganyika na mimea ya ardhi wanayo ila watu na wanyama. Mpaka ardhi ilipo kamilika uzuri wake, na ikapambika, na wenyewe wakadhani wamesha iweza, iliifikia amri yetu usiku au mchana, tukaifanya kama iliyo fyekwa - kama kwamba haikuwapo jana. Namna hivi tunazipambanua Ishara zetu kwa watu wanao fikiri.
(25) Na Mwenyezi Mungu anaita kwendea Nyumba ya Amani, na anamwongoa amtakaye kwenye Njia Iliyo Nyooka.