(191) Na wauweni popote mwakutapo, na muwatoe popote walipo kutoeni; kwani fitina ni mbaya zaidi kuliko kuuwa. Wala msipigane nao kwenye Msikiti Mtakatifu mpaka wakupigeni huko. Wakikupigeni huko basi nanyi pia wapigeni. Na hivi ndivyo yalivyo malipo ya makafiri.
(192) Lakini wakiacha basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
(193) Na piganeni nao mpaka pasiwepo fitina, na Dini iwe ya Mwenyezi Mungu tu. Na kama wakiacha basi usiweko uadui ila kwa wenye kudhulumu.
(194) Mwezi mtakatifu kwa mwezi mtakatifu. Na vitu vitakatifu vimeekewa kisasi. Anaye kushambulieni nanyi mshambulieni, kwa kadiri alivyo kushambulieni. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachamngu.
(195) Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo. Na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.
(196) Na timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa mkizuiwa, basi (chinjeni) wanyama walio wepesi kupatikana. Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama hao wafike machinjoni mwao. Na atakaye kuwa mgonjwa au ana vya kumuudhi kichwani mwake basi atoe fidiya kwa kufunga au kwa kutoa sadaka au kuchinja wanyama. Na mtakapo kuwa salama, basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha ndio akahiji, basi achinje mnyama aliye mwepesi kumpata. Na asiye pata, afunge siku tatu katika Hija na siku saba mtakapo rudi; hizi ni kumi kaamili. Hayo ni kwa ajili ya yule ambaye watu wake hawako karibu na Msikiti Mtakatifu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.