(118) Na pia wale watatu walio achwa nyuma hata dunia wakaiona dhiki juu ya ukunjufu wake, na nafsi zao zikabanika, na wakayakinika kuwa hapana pa kumkimbia Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwake Yeye. Kisha akawaelekea kwa rehema yake ili nao waendelee kutubu. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu.
(119) Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kuweni pamoja na wakweli.
(120) Haiwafalii watu wa Madina na Mabedui walio jirani zao kubakia nyuma wasitoke na Mtume, wala kujipendelea nafsi zao kuliko yeye. Hayo ni kwa kuwa hakiwapati kiu, wala machofu, wala njaa, kwa ajili ya Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawendi mahali panapo waghadhibisha makafiri, wala hakiwapati chochote kutokana na maadui, ila huandikiwa kuwa ni kitendo chema. Hakika Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa wanao fanya mema.
(121) Wala hawatoi cha kutoa kidogo wala kikubwa, wala hawalivuki bonde, ila huandikiwa, ili Mwenyezi Mungu awalipe bora ya waliyo kuwa wakiya- tenda.
(122) Wala haiwafalii Waumini kutoka wote. Lakini kwa nini hawatoki baadhi katika kila kundi miongoni mwao, wakajifunze vyema Dini, na kisha waje kuwaonya wenzao watakapo warejea, ili wapate kujihadharisha?