التوبة At-Tawba
(1) Huku ni kujitoa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwenye jukumu la maagano na mlio ahidiana nao katika washirikina.
(2) Basi tembeeni katika nchi miezi mine, na jueni kwamba nyinyi hamwezi kumshinda Mwenyezi Mung, na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anaye wahizi makafiri.
(3) Na ni tangazo kutokana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa wote siku ya Hija Kubwa kwamba Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawana jukumu lolote kwa washirikina. Basi mkitubu itakuwa kheri kwenu, na mkigeuka basi jueni kuwa nyinyi hamumshindi Mwenyezi Mungu. Na wabashirie makafiri kuwa watapata adhabu chungu.
(4) Isipo kuwa washirikina ambao mliahidiana nao kisha wasikupunguzieni chochote, wala hawakumsaidia yeyote dhidi yenu, basi hao watimizieni ahadi yao mpaka muda wao. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wacha-Mungu.
(5) Na ikisha miezi mitukufu basi wauweni washirikina popote mwakutapo, na washikeni na wazungukeni, na wavizieni katika kila njia. Lakini wakitubu, wakashika Sala, na wakatoa Zaka, basi waachilieni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
(6) Na ikiwa mmoja wapo katika washirikina akikuomba ulinzi, basi mpe ulinzi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu. Kisha mfikishe pahala pake pa amani. Haya ni kwa kuwa hao ni watu wasiojua kitu.