(10) Na wale walio kufuru na wakakanusha Ishara zetu, hao ndio watu wa Motoni.
(11) Enyi mlio amini! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu, walipo taka watu kukunyooshieni mikono, naye akaizuilia mikono yao kukufikieni. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu.
(12) Na Mwenyezi Mungu alifanya agano na Wana wa Israili. Na tukawateulia kutokana nao wakuu kumi na mbili. Na Mwenyezi Mungu akasema: Kwa yakini Mimi ni pamoja nanyi. Mkisali, na mkatoa Zaka, na mkawaamini Mitume wangu, na mkawasaidia, na mkamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, hapana shaka nitakufutieni maovu yenu na nitakuingizeni katika mabustani yapitayo mito kati yake. Lakini atakaye kufuru miongoni mwenu baada ya hayo bila ya shaka atakuwa amepotea njia iliyo sawa.
(13) Basi kwa sababu ya kuvunja agano lao tuliwalaani, na tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu. Wanayabadilisha maneno kutoka pahala pake, na wamesahau sehemu ya yale waliyo kumbushwa. Na huachi kuvumbua khiana kutokana nao, isipo kuwa wachache miongoni mwao. Basi wasamehe na waache. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.