(6) Na Musa alipo waambia watu wake: Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu aliyo kujaalieni, pale alipo kuokoeni kutokana na watu wa Firauni walio kupeni adhabu mbaya kabisa, wakiwachinja wenenu wanaume, na wakiwawacha hai wanawake. Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa unao toka kwa Mola wenu Mlezi.
(7) Na alipo tangaza Mola wenu Mlezi: Mkishukuru nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.
(8) Na Musa alisema: Mkikufuru nyinyi na wote waliomo duniani, hakika Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Anajitosha, Msifiwa.
(9) Je! Hazikukufikieni khabari za walio kabla yenu? Kaumu ya Nuhu, na A'adi, na Thamud, na walio baada yao, ambao hapana awajuaye ila Mwenyezi Mungu? Mitume wao waliwajia kwa hoja zilizo wazi, na wao wakarudisha mikono yao kwenye vinywa vyao, wakasema: Hakika sisi tumeyakataa hayo mliyo tumwa, na hakika sisi tuna shaka kubwa na mnayo tuitia.
(10) Mitume wao wakasema: Ati pana shaka na Mwenyezi Mungu, Muumba mbingu na ardhi? Yeye anakuiteni apate kukufutieni madhambi yenu, na akupeni muhula mpaka muda ulio wekwa. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni wanaadamu kama sisi. Mnataka kutuzuilia na waliyo kuwa wakiabudu baba zetu. Basi tuleteeni hoja ilio wazi.