(37) Watataka watoke Motoni, lakini hawatatoka humo, na watakuwa na adhabu inayo dumu.
(38) Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao, hayo ni malipo ya waliyo yachuma, ndiyo adhabu ya mfano itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
(39) Lakini mwenye kutubia baada ya dhulma yake, na akatengenea, basi Mwenyezi Mungu atapokea toba yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.
(40) Hujui ya kwamba Mwenyezi Mungu anao ufalme wa mbingu na ardhi? Humuadhibu amtakaye, na humsamehe amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
(41) Ewe Mtume! Wasikuhuzunishe wa fanyao haraka kukufuru, miongoni mwa wanao sema kwa vinywa vyao: Tumeamini, na hali nyoyo zao hazikuamini, na miongoni mwa Mayahudi, wanao sikiliza kwa ajili ya uwongo, wanao sikiliza kwa ajili ya watu wengine wasio kufikia. Wao huyabadilisha maneno kutoka pahala pake. Wanasema: Mkipewa haya basi yashikeni, na msipo pewa haya tahadharini. Na mtu ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumfitini huwezi kuwa na madaraka naye mbele ya Mwenyezi Mungu. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu hataki kuzitakasa nyoyo zao. Watakuwa na hizaya duniani, na Akhera watakuwa na adhabu kubwa.