(171) Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msimseme Mwenyezi Mungu ila kwa lilio kweli. Hakika Masihi Isa mwana wa Maryamu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilo mpelekea Maryamu, na ni roho iliyo toka kwake. Basi Muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Wala msiseme: Utatu. Komeni! Itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ametukuka Yeye na kuwa na mwana. Ni vyake Yeye vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa kutosha.
(172) Masihi hataona uvunjifu kuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu, wala Malaika walio karibishwa. Na watakao ona uvunjifu utumwa wa Mwenyezi Mungu na kufanya kiburi, basi atawakusanya wote kwake.
(173) Na ama walio amini na wakatenda mema atawalipa ujira wao sawa sawa, na atawazidishia kwa fadhila yake. Na ama wale walio ona uvunjifu na wakafanya kiburi, basi atawaadhibu adhabu iliyo chungu. Wala hawatopata mlinzi wala wa kuwanusuru asiye kuwa Mwenyezi Mungu.
(174) Enyi watu! Umekufikieni ushahidi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na tumekuteremshieni Nuru iliyo wazi.
(175) Ama wale walio muamini Mwenyezi Mungu, na wakashikamana naye, basi atawatia katika rehema yake na fadhila, na atawaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka.