(89) Watakao kuja na mema, watapata bora kuliko hayo. Nao watasalimika na mahangaiko ya Siku hiyo.
(90) Na watakao kuja na uovu, basi zitasunukishwa nyuso zao Motoni. Je! Kwani mnalipwa isipo kuwa mliyo kuwa mkiyatenda?
(91) Ama mimi nimeamrishwa nimuabudu Mola Mlezi wa mji huu aliye ufanya ni mtakatifu; na ni vyake Yeye tu vitu vyote. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa Waislamu, wenye kunyenyekea.
(92) Na niisome Qur'ani. Na mwenye kuongoka, basi ameongoka kwa faida ya nafsi yake; na aliye potea - basi sema: Hakika mimi ni miongoni mwa waonyaji.
(93) Na sema: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Yeye atakuonyesheni Ishara zake, na mtazijua. Na Mola wako Mlezi si mwenye kughafilika na myatendayo.
القصص Al-Qasas
(1) T'A SIN MIM, (T'. S. M.)
(2) Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha.
(3) Tunakusomea khabari za Musa na Firauni kwa Haki kwa ajili ya watu wanao amini.
(4) Hakika Firauni alitakabari katika nchi, na akawagawa wananchi makundi mbali mbali. Akalidhoofisha taifa moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wanaume na akiwaacha watoto wao wanawake. Hakika yeye alikuwa katika mafisadi.
(5) Na tukataka kuwafadhili walio dhoofishwa katika nchi hiyo na kuwafanya wawe waongozi na kuwafanya ni warithi.