(23) Hakika mimi nimemkuta mwanamke anawatawala, naye amepewa kila kitu, na anacho kiti cha enzi kikubwa.
(24) Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi Mungu; na Shet'ani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia Njia. Kwa hivyo hawakuongoka,
(25) Na hawamsujudii Mwenyezi Mungu ambaye huyatoa yaliyo fichikana katika mbingu na ardhi, na anayajua mnayo yaficha na mnayo yatangaza.
(26) Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa A'rshi tukufu..
(27) Akasema (Sulaiman): Tutatazama umesema kweli au wewe ni miongoni mwa waongo.
(28) Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha waache na utazame watarejesha nini.
(29) (Malkia) akasema: Enyi wahishimiwa! Hakika nimeletewa barua tukufu.
(30) Imetoka kwa Sulaiman nayo ni: Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
(31) Msinifanyie jeuri, na fikeni kwangu nanyi mmekwisha kuwa wenye kusalimu amri.
(32) Akasema: Enyi wahishimiwa! Nipeni shauri katika jambo langu hili, kwani mimi sikati shauri yoyote mpaka mhudhurie.
(33) Wakasema: Sisi ni wenye nguvu na wakali kwa vita; na amri iko kwako, basi tazama ni nini unaamrisha.
(34) Akasema: Hakika wafalme wanapo uingia mji wanauharibu, na wanawafanya wale watukufu wake kuwa wanyonge. Na hivyo ndivyo watendavyo.
(35) Lakini mimi nitawapelekea zawadi, nami nitangoja watakayo rudi nayo wajumbe.