النور An-Noor
(1) HII NI SURA Tuliyo iteremsha na tukailazimisha; tukateremsha ndani yake Aya zilizo wazi ili mkumbuke.
(2) Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini.
(3) Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina. Na mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina. Na hayo yameharimishwa kwa Waumini.
(4) Na wanao wasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete mashahidi wane, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio wapotovu.
(5) Isipo kuwa wale walio tubu baada ya hayo na wakatengenea; kwani bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye kurehemu.
(6) Na wale wanao wasingizia wake zao na hawana mashahidi ila nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudilia mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba hakika yeye ni katika wasema kweli.
(7) Na mara ya tano kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake ikiwa ni miongoni mwa waongo.
(8) Na mke itamwondokea adhabu kwa kutoa shahada mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba huyu mume ni miongoni mwa waongo.
(9) Na mara ya tano ya kwamba ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake kama mumewe yu miongoni mwa wanao sema kweli.
(10) Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, na ya kuwa Mwenyezi Mungu ni Mpokeaji toba....