(73) Na tukawafanya maimamu wakiongoa watu kwa amri yetu. Na tukawafunulia watende kheri, na washike Sala, na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi tu.
(74) Na Luut'i tukampa hukumu na ilimu na tukamwokoa na ule mji ulio kuwa ukifanya maovu. Hakika hao walikuwa watu wabaya, wachafu.
(75) Na tukamuingiza katika rehema yetu. Hakika yeye ni miongoni mwa watenda mema.
(76) Na Nuhu alipo ita zamani, nasi tukamuitikia, na tukamwokoa yeye na watu wake kutokana na shida kubwa.
(77) Na tukamnusuru na watu walio zikanusha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu wabaya. Basi tukawazamisha wote.
(78) Na Daud na Suleiman walipo kata hukumu katika kadhiya ya konde walipo lisha humo mbuzi wa watu usiku. Na Sisi tulikuwa wenye kushuhudia hukumu yao hiyo.
(79) Tukamfahamisha Suleiman. Na kila mmoja wao tulimpa hukumu na ilimu. Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee na imtakase Mwenyezi Mungu. Na Sisi ndio tulio fanya hayo.
(80) Na tukamfundisha kuunda mavazi ya vita kwa ajili yenu ili yakuhifadhini katika kupigana kwenu. Je! Mtakuwa wenye kushukuru?
(81) Na tukamsahilishia Suleiman upepo wa kimbunga wendao kwa amri yake kwenye ardhi tuliyo ibarikia. Na Sisi ndio tunao jua kila kitu.