(20) Kwani hamwoni ya kwamba Mwenyezi Mungu amevifanya vikutumikieni viliomo mbinguni na kwenye ardhi, na akakujalizieni neema zake, za dhaahiri na za siri? Na miongoni mwa watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu pasipo ilimu, wala uwongofu, wala Kitabu chenye nuru.
(21) Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, husema: Bali tunafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je! Ijapo kuwa Shet'ani anawaita kwenye adhabu ya Moto uwakao?
(22) Na mwenye kuuelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye akawa anafanya wema, basi huyo hakika amekwisha kamata fundo lilio madhubuti. Na mwisho wa mambo yote ni kwa Mwenyezi Mungu.
(23) Na anaye kufuru, isikuhuzunishe kufuru yake. Kwetu ndio marudio yao, na hapo tutawaambia waliyo yatenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
(24) Tunawastarehesha kwa uchache, kisha tutawasukuma kwenye adhabu ngumu.
(25) Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Mwenyezi Mungu. Wewe sema: Alhamdulillahi! Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.
(26) Ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo mbinguni na katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mkwasi, Mwenye kusifiwa.
(27) Na lau kuwa miti yote iliyomo duniani ikawa ni kalamu, na bahari (ikawa wino), na ikaongezewa juu yake bahari nyengine saba, maneno ya Mwenyezi Mungu yasingeli kwisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
(28) Hakukuwa kuumbwa kwenu, wala kufufuliwa kwenu ila ni kama nafsi moja tu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.