(170) Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu; wao husema: Bali tutafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je, hata ikiwa baba zao walikuwa hawaelewi kitu, wala hawakuongoka?
(171) Na mfano wa walio kufuru ni kama mfano wa anaye mpigia kelele asiye sikia ila wito na sauti tu -- ni viziwi, mabubu, vipofu, kwa hivyo hawaelewi.
(172) Enyi mlio amini! Kuleni vizuri tulivyo kuruzukuni, na mumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli mnamuabudu Yeye tu.
(173) Yeye amekuharimishieni mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilicho tajiwa, katika kuchinjwa kwake, jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu. Lakini aliye fikiwa na dharura bila ya kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(174) Hakika wale wafichao aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu katika Kitabu, wakanunua kwacho thamani ndogo, hao hawali matumboni mwao isipo kuwa moto, wala Mwenyezi Mungu hatawasemeza Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa. Nao watapata adhabu chungu.
(175) Hao ndio walio nunua upotofu badala ya uwongofu, na adhabu badala ya maghfira. Ama wavumilivu wa Moto watu hawa!
(176) Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameteremsha Kitabu kwa haki. Na wale walio khitilafiana katika Kitabu wamo katika upinzani ulio mbali na haki.