(135) Na wakasema: Kuweni Mayahudi au Wakristo ndio mtaongoka. Sema: Bali tunashika mila ya Ibrahim mwongofu, wala hakuwa katika washirikina.
(136) Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyo teremshiwa sisi, na yaliyo teremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na wajukuu zake, na waliyo pewa Musa na Isa, na pia waliyo pewa Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutafautishi baina ya yeyote katika hao, na sisi tumesilimu kwake.
(137) Basi wakiamini kama mnavyo amini nyinyi, itakuwa kweli wameongoka. Na wakikengeuka basi wao wamo katika upinzani tu. Na Mwenyezi Mungu atakutosheni kukukingeni na shari yao, na Yeye ndiye Msikizi, Mjuzi.
(138) Huko ndiko kupaka rangi kwa Mwenyezi Mungu, na nani aliye mbora wa kupaka rangi kuliko Mwenyezi Mungu? Na sisi ni wenye kumuabudu Yeye tu.
(139) Sema: Mnahojiana nasi juu ya Mwenyezi Mungu, naye ni Mola wetu Mlezi na Mola wenu Mlezi, na sisi tuna vitendo vyetu na nyinyi mna vitendo vyenu? Nasi tunamsafia Yeye tu.
(140) Au mnasema kuwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na wajukuu zao walikuwa Mayahudi au Wakristo? Sema: Je, nyinyi mnajua zaidi au Mwenyezi Mungu? Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule aliye ficha ushahidi alio nao utokao kwa Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na hayo myafanyayo.
(141) Hao ni watu walio kwisha pita. Wao watapata waliyo yachuma, na nyinyi mt apata mliyo yachuma, wala hamtaulizwa nyinyi yale waliyo kuwa wakifanya wao.