(84) Na tulipo chukua agano lenu kuwa hamtamwaga damu zenu, wala hamtatoana majumbani mwenu; nanyi mkakubali nanyi mnashuhudia.
(85) Kisha nyinyi kwa nyinyi mnauwana, na mnawatoa baadhi yenu majumbani kwao, mkisaidiana kwa dhambi na uadui. Na wakikujieni mateka mnawakomboa, na hali kuwatoa mmekatazwa. Je! Mnaamini baadhi ya Kitabu na mnakataa baadhi yake? Basi hana malipo mwenye kutenda hayo miongoni mwenu ila hizaya katika maisha ya duniani, na Siku ya Kiyama watapelekwa kwenye adhabu kali kabisa. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale mnayo yatenda.
(86) Hao ndio walio nunua uhai wa dunia kwa (uhai wa) Akhera; kwa hivyo hawatapunguziwa adhabu wala hawatanusuriwa.
(87) Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukafuatisha baada yake Mitume wengine. Na tukampa Isa, mwana wa Mariamu, hoja zilizo waziwazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Basi kila walipo kufikieni Mitume kwa yale ambayo hayapendwi na nafsi zenu, mlijivuna; wengine mkawakanusha, na wengine mkawauwa.
(88) Na walisema: Nyoyo zetu zimefunikwa. Bali Mwenyezi Mungu amewalaani kwa kufuru zao: kwa hivyo ni kidogo tu wanayo yaamini.