(25) Na katika Ishara zake ni kuwa mbingu na ardhi zimesimama kwa amri yake. Kisha atakapo kuiteni mwito mmoja tu, hapo mtatoka kwenye ardhi.
(26) Na vyake Yeye vilivyo mbinguni na katika ardhi. Vyote vinamt'ii Yeye.
(27) Na Yeye ndiye anaye anzisha uumbaji, kisha ataurudisha mara nyengine. Na jambo hili ni jepesi zaidi kwake. Naye ndiye mwenye mfano bora katika mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
(28) Amekupigieni mfano kutokana na nafsi zenu. Je! Katika hao iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia mnao washirika katika hivyo tulivyo kuruzukuni, mkawa nyinyi katika hivyo ni sawasawa, mnawaogopa kama mnavyo ogopana wenyewe kwa wenyewe? Namna hivi tunazipambanua Aya zetu kwa watu wenye akili.
(29) Bali walio dhulumu wamefuata mapendo ya nafsi zao pasina kujua. Basi nani atamwongoa ambaye Mwenyezi Mungu amemuacha apotee? Wala hao hawatakuwa na wa kuwanusuru.
(30) Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini - ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilo waumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyo nyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui.
(31) Muwe wenye kutubia kwake, na mcheni Yeye, na shikeni Sala, na wala msiwe katika washirikina.
(32) Katika wale ambao kwamba wameigawanya dini yao, na wakawa makundi makundi, kila kikundi kinafurahia kilicho nacho.