(187) Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu anajua kwamba mlikuwa mkizikhini nafsi zenu. Kwa hivyo amekukubalieni toba yenu na amekusameheni. Basi sasa changanyikeni nao na takeni aliyo kuandikieni Mwenyezi Mungu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikaribie. Namna hivi Mwenyezi Mungu anabainisha Ishara zake kwa watu ili wapate kumcha.
(188) Wala msiliane mali zenu kwa baat'ili na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi, na hali mnajua.
(189) Wanakuuliza khabarai ya miezi. Sema: Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa ajili ya watu na Hija. Wala sio wema kuziingia nyumba kwa nyuma. Bali mwema ni mwenye kuchamngu. Na ingieni majumbani kupitia milangoni. Na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa.
(190) Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanao kupigeni, wala msianze uadui. Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi waanzao uadui.