(143) Amekuumbieni namna nane za wanyama: Wawili katika kondoo, na wawili katika mbuzi. Sema je, ameharimisha yote madume wawili au majike wawili, au waliomo matumboni mwa majike yote mawili? Niambieni kwa ilimu ikiwa nyinyi mnasema kweli.
(144) Na wawili katika ngamia, na wawili katika ng'ombe. Sema: Je, ameharimisha yote madume wawili au majike wawili, au waliomo matumboni mwa yote majike? Au, nyinyi mlikuwapo Mwenyezi Mungu alipo kuusieni haya? Basi ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule aliye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, kwa ajili ya kuwapoteza watu bila ya ilimu? Hakika Mwenyezi Mungu hawahidi watu madhaalimu.
(145) Sema: Sioni katika yale niliyo funuliwa mimi kitu kilicho harimishwa kwa mlaji kukila isipo kuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayo mwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu; au kwa upotofu kimechinjwa kwa jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu. Lakini mwenye kushikwa na dharura, bila ya kutamani wala kupita mipaka, basi hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(146) Na wale walio fuata dini ya Kiyahudi tumewaharimishia kila mwenye kucha. Na katika ng'ombe na kondoo na mbuzi tumewaharimishia shahamu yao, isipo kuwa ile iliyo beba migongo yao au matumbo yao, au iliyo gandamana na mifupa. Tuliwalipa hivyo kwa sababu ya uasi wao. Na bila ya shaka Sisi ndio wasema kweli.