(54) Na lau kuwa kila nafsi iliyo dhulumu inamiliki kila kiliomo duniani, bila ya shaka ingeli toa vyote kujikombolea. Na watakapo iona adhabu wataficha majuto. Na patahukumiwa baina yao kwa uadilifu, nao hawatadhulumiwa.
(55) Jueni kuwa hakika vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi ni vya Mwenyezi Mungu. Jueni kuwa hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Lakini wengi wao hawajui.
(56) Yeye ndiye anaye fufua na anaye fisha. Na kwake mtarejeshwa.
(57) Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uwongofu, na rehema kwa Waumini.
(58) Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake! Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayo yakusanya.
(59) Sema: Je! Mwaonaje zile riziki alizo kuteremshieni Mwenyezi Mungu, nanyi mkafanya katika hizo nyengine haramu na nyengine halali. Sema: Je! Mwenyezi Mungu amekuruhusuni, au mnamzulia Mwenyezi Mungu tu?
(60) Na nini dhana ya wanao mzulia Mwenyezi Mungu kwa Siku ya Kiyama? Hakika Mwenyezi Mungu ana fadhila juu ya watu, lakini wengi wao hawashukuru.
(61) Na huwi katika jambo lolote, wala husomi sehemu yoyote katika Qur'ani, wala hamtendi kitendo chochote ila Sisi huwa ni mashahidi juu yenu mnapo shughulika nayo. Na hakifichikani kwa Mola wako Mlezi chenye uzito hata wa chembe katika ardhi na katika mbingu, wala kidogo kuliko hicho wala kikubwa ila kimo katika Kitabu kilicho wazi.