(38) Na akawa anaunda jahazi, na kila wakipita wakuu wa kaumu yake wakimkejeli. Yeye akasema: Ikiwa nyinyi mnatukejeli na sisi tunakukejelini kama mnavyo tukejeli.
(39) Nanyi mtakuja jua ni nani itakaye mfikia adhabu ya kumhizi, na itakaye mteremkia adhabu ya kudumu.
(40) Hata ilipo kuja amri yetu, na tanuri ikafoka maji, tulisema: Pakia humo wawili wawili, dume na jike, kutoka kila aina, na ahali zako, isipo kuwa wale ambao imekwisha wapitia hukumu; na watu walio amini. Na hawakuamini pamoja naye ila wachache tu.
(41) Na akasema: Pandeni humo kwa Bismillahi, Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, kwenda kwake na kusimama kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
(42) Ikawa inakwenda nao katika mawimbi kama milima. Na Nuhu akamwita mwanawe naye alikuwa mbali: Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi, wala usiwe pamoja na makafiri.
(43) Akasema: Nitakimbilia mlimani unilinde na maji. (Nuhu) akasema: Leo hapana wa kulindwa na amri ya Mwenyezi Mungu ila aliye mrehemu mwenyewe. Na wimbi likawatenganisha, akawa katika walio zama.
(44) Na ikasemwa: Ewe ardhi! Meza maji yako. Na Ewe mbingu! Jizuie. Basi maji yakadidimia chini, na amri ikapitishwa, na (jahazi) likasimama juu ya (mlima) wa Al Juudiy. Na ikasemwa: Wapotelee mbali watu walio dhulumu!
(45) Na Nuhu alimwomba Mola wake Mlezi: Ee Mola Mlezi wangu! Hakika mwanangu ni katika ahali zangu, na hakika ahadi yako ni haki. Na Wewe ni Mwenye haki kuliko mahakimu wote.