(25) Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka.
(26) Na mfano wa neno ovu ni kama mti muovu, ulio ng'olewa juu ya ardhi. Hauna imara.
(27) Mwenyezi Mungu huwatia imara wenye kuamini kwa kauli ya imara katika maisha ya dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwaacha kupotea hao wenye kudhulumu. Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo.
(28) Hebu hukuwaona wale walio badilisha neema ya Mwenyezi Mungu kwa kufuru, na wakawafikisha watu wao kwenye nyumba ya maangamizo?
(29) Nayo ni Jahannamu! Maovu yaliyoje makaazi hayo!
(30) Na walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili wapoteze watu kwenye Njia yake. Sema: Stareheni! Kwani marejeo yenu ni Motoni!
(31) Waambie waja wangu walio amini, washike Sala, na watoe katika tulivyo waruzuku, kwa siri na dhaahiri, kabla haijafika Siku isiyo kuwa na biashara wala urafiki.
(32) Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi, na akateremsha maji kutoka mbinguni. Na kwa hayo akatoa matunda kuwa ni riziki yenu. Na akafanya yakutumikieni majahazi yanayo pita baharini kwa amri yake, na akaifanya mito ikutumikieni.
(33) Na akalifanya jua na mwezi kwa manufaa yenu daima dawamu, na akaufanya usiku na mchana kwa manufaa yenu.