(97) Na anaye mhidi Mwenyezi Mungu basi huyo ndiye aliye hidika. Na anaye wapotoa basi huto wapatia walinzi badala yake. Na tutawakusanya Siku ya Kiyama hali wakikokotwa juu ya nyuso zao, nao ni vipofu na mabubu na viziwi. Na makaazi yao ni Jahannamu. Kila moto ukifanya kusinzia tutazidi kuuchochea uwake kwa nguvu.
(98) Hayo ni malipo yao kwa sababu walizikataa ishara zetu, na wakasema: Hivyo tukisha kuwa mifupa na mapande yaliyo vurugika tutafufuliwa kwa umbo jipya?
(99) Kwani hawakuona ya kwamba Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi ni Mwenye kuweza kuumba mfano wao? Na Yeye amewawekea muda usio na shaka yoyote. Lakini madhaalimu hawataki ila ukafiri.
(100) Sema: Lau kuwa nyinyi mnazimiliki khazina za rehema za Mola wangu Mlezi, basi hapana shaka mngeli zuia kuzitumia kwa ajili ya kukhofu. Na mwanaadamu tangu hapo tabia yake ni mchoyo!
(101) Na kwa yakini tulimpa Musa ishara tisa zilizo wazi. Waulize Wana wa Israili alipo wafikia, na Firauni akawaambia: Hakika mimi nakuona wewe Musa umerogwa!
(102) Musa akasema: Wewe unajua bila ya shaka kuwa haya hakuyateremsha ila Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ili kuwa ni ushahidi wa kuonekana. Na hakika mimi bila ya shaka nakuona wewe, Firauni, kuwa umekwisha angamia.
(103) Basi Firauni akataka kuwafukuza katika nchi. Kwa hivyo tukamzamisha yeye na walio kuwa pamoja naye wote.
(104) Na tukawaambia baada yake Wana wa Israili: Kaeni katika nchi. Itapo kuja ahadi ya Akhera tutakuleteni nyote pamoja.