(26) Basi kula, na kunywa, na litue jicho lako. Na pindi ukimwona mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu ya kufunga; kwa hivyo leo sitasema na mtu.
(27) Akenda naye (mwanawe) kwa jamaa zake amembeba. Wakasema: Ewe Maryamu! Hakika umeleta kitu cha ajabu!
(28) Ewe dada yake Harun! Baba yako hakuwa mtu muovu, wala mama yako hakuwa kahaba.
(29) Akawaashiria (mtoto). Wakasema: Vipi tumsemeze aliye bado mdogo yumo katika mlezi?
(30) (Mtoto) akasema: Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu. Amenipa Kitabu, na amenifanya Nabii.
(31) Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo. Na ameniusia Sala na Zaka maadamu ni hai,
(32) Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri, mwovu.
(33) Na amani iko juu yangu siku niliyo zaliwa, na siku nitakayo kufa, na siku nitakayo fufuliwa kuwa hai.
(34) Huyo ndiye Isa mwana wa Maryamu. Ndiyo kauli ya haki ambayo wanaifanyia shaka.
(35) Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwa na mwana, Subhanahu, Yeye ametakasika! Anapo lihukumia jambo basi huliambia tu: Kuwa! Likawa.
(36) Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
(37) Lakini makundi yakakhitalifiana wao kwa wao. Basi ole wao hao walio kufuru kwa kuhudhuria Siku iliyo kuu!
(38) Watasikia na wataona vizuri vilioje Siku watakayo tufikia! Lakini madhaalimu sasa wamo katika upotofu ulio dhaahiri.