(32) Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye kujua.
(33) Na wajizuilie na machafu wale wasio pata cha kuolea, mpaka Mwenyezi Mungu awatajirishe kwa fadhila yake. Na wanao taka kuandikiwa uhuru katika wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki, basi waandikieni kama mkiona wema kwao. Na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu aliyo kupeni. Wala msiwashurutishe vijakazi vyenu kufanya zina kwa ajili ya kutafuta pato la maisha ya dunia, ilhali wao wanataka kujihishimu. Na atakaye walazimisha basi Mwenyezi Mungu baada ya kulazimishwa kwao huko, atawasamehe, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(34) Na kwa yakini tumekuteremshieni Ishara zilizo wazi na mifano kutokana na walio tangulia kabla yenu na mawaidha kwa wachamngu.
(35) Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru yake ni kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa ile imo katika tungi. Tungi lile ni kama nyota inayo meremeta, inayo washwa kwa mafuta yanayo toka katika mti ulio barikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakaribia mafuta yake kung'aa wenyewe ingawa moto haujayagusa - Nuru juu ya Nuru. Mwenyezi Mungu humwongoa kwenye Nuru yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
(36) Katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na humo litajwe jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni