(60) Na chochote mlicho pewa ni matumizi ya maisha ya dunia na pambo lake. Na yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ndio bora na yatakayo baki zaidi. Basi je, hamfahamu?
(61) Je! Yule tuliye muahidi ahadi nzuri, tena naye akayapata, ni kama tuliye mstarehesha kwa starehe za maisha ya duniani, na kisha Siku ya Kiyama akawa miongoni mwa wanao hudhurishwa?
(62) Na siku atakapo waita na akasema: Wako wapi mlio kuwa mkidai kuwa ni washirika wangu?
(63) Watasema wale iliyo thibiti juu yao kauli: Mola wetu Mlezi! Hawa ndio tulio wapoteza. Tuliwapoteza kama tulivyo potea sisi. Tunajitenga nao mbele yako. Hawakuwa wakituabudu sisi.
(64) Na itasemwa: Waiteni hao miungu wa kishirikina wenu! Basi watawaita, lakini hawatawaitikia, na wataiona adhabu; laiti wangeli kuwa wameongoka!
(65) Na siku atapo waita na akasema: Mliwajibu nini Mitume?
(66) Basi zitawapotea khabari siku hiyo, nao hawataulizana.
(67) Ama mwenye kutubu na akaamini na akatenda mema, huyo atakuwa miongoni mwa wenye kufanikiwa.
(68) Na Mola wako Mlezi huumba na huteuwa atakavyo. Viumbe hawana khiari. Mwenyezi Mungu ametukuka na ametakasika na hao wanao washirikisha naye.
(69) Na Mola wako Mlezi anayajua yaliyo ficha vifua vyao, na wanayo yatangaza.
(70) Naye ni Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye. Sifa zote njema ni zake Yeye, mwanzo na mwisho. Na hukumu ni yake Yeye. Na kwake Yeye mtarejeshwa.