(6) Ni ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji ahadi yake. Lakini watu wengi hawajui.
(7) Wanajua hali ya dhaahiri ya maisha ya dunia, na wameghafilika na Akhera.
(8) Je! Hawajifikirii nafsi zao? Mwenyezi Mungu hakuumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yake ila kwa Haki na kwa muda maalumu. Na hakika watu wengi bila ya shaka ni wenye kukataa kuwa watakutana na Mola wao Mlezi.
(9) Je! Hawatembei katika ardhi wakaona ulivyo kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Nao walikuwa na nguvu zaidi kuliko wao, na wakaitimbua ardhi na wakaistawisha zaidi kuliko walivyo istawisha wao. Na Mitume wao wakawajia na dalili zilizo wazi. Basi hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wakijidhulumu nafsi zao.
(10) Kisha ulikuwa mwisho wa walio fanya ubaya ni kuzikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakawa wanazifanyia maskhara.
(11) Mwenyezi Mungu huanzisha uumbaji, tena akaurudisha mara ya pili, na kisha mtarejeshwa kwake.
(12) Na itapo simama Saa wakosefu watakata tamaa.
(13) Wala hawatakuwa na waombezi miongoni mwa walio kuwa wakiwashirikisha na Mungu; na wao wenyewe watawakataa hao washirikishwa wao.
(14) Na siku itapo simama Saa, siku hiyo watagawanyika.
(15) Ama walio amini na wakatenda mema watafurahishwa katika Bustani.