(12) Na ungeli waona wakosefu wanvyo inamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao Mlezi, (wakisema): Mola wetu Mlezi! Tumesha ona, na tumesha sikia. Turejeshe tukatende mema, kwani hakika sisi tumekwisha kuwa na yakini sasa.
(13) Na lau tungeli taka tunge mpa kila mtu uwongofu wake. Lakini imekwisha kuwa kauli iliyo toka kwangu: Kwa yakini nitaijaza Jahannamu kwa wote hawa, majini na watu.
(14) Basi onjeni kwa vile mlivyo usahau mkutano wa Siku yenu hii. Na Sisi hakika tunakusahauni. Basi onjeni adhabu ya milele kwa yale mliyo kuwa mkiyatenda.
(15) Hakika wanao ziamini Aya zetu ni hao tu ambao wakikumbushwa hizo, basi wao huanguka kusujudu, na humsabihi Mola wao Mlezi kwa kumhimidi, nao hawajivuni.
(16) Mbavu zao zinaachana na vitanda kwa kumwomba Mola wao Mlezi kwa khofu na kutumaini, na hutoa kutokana na tulivyo waruzuku.
(17) Nafsi yoyote haijui waliyo fichiwa katika hayo yanayo furahisha macho - ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyatenda.
(18) Ati aliye Muumini atakuwa sawa na aliye mpotovu? Hawawi sawa.
(19) Ama walio amini na wakatenda mema, watakuwa nazo Bustani za makaazi mazuri. Ndio pa kufikia kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
(20) Na ama wale walio tenda uovu, basi makaazi yao ni Motoni. Kila wakitaka kutoka humo watarudishwa humo humo. Na wataambiwa: Onjeni adhabu ya Moto ambayo mliyo kuwa mkiikanusha.