(48) Na utawadhihirikia ubaya wa waliyo yachuma, yatawazunguka waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha.
(49) Na dhara inapo mgusa mtu hutuomba. Kisha tunapo mpa neema zitokazo kwetu, husema: Nimepewa haya kwa sababu ya ilimu yangu. Sio! Huo ni mtihani! Lakini wengi wao hawajui!
(50) Waliyasema haya waliyo kuwa kabla yao, lakini hayakuwafaa waliyo kuwa wakiyachuma.
(51) Basi ukawasibu uovu wa waliyo yachuma. Na wale walio dhulumu miongoni mwa hawa utawasibu uovu wa waliyo yachuma vile vile. Nao si wenye kushinda.
(52) Kwani wao hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na akamkadiria? Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao amini.
(53) Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(54) Na rejeeni kwa Mola wenu Mlezi, na silimuni kwake, kabla ya kukujieni adhabu. Kisha hapo hamtanusuriwa.
(55) Na fuateni yaliyo bora kabisa katika yale yaliyo teremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu Mlezi, kabla haijakujieni adhabu kwa ghafla, na hali hamtambui.
(56) Isije ikasema nafsi: Ee majuto yangu kwa yale niliyo poteza upande wa Mwenyezi Mungu, na hakika nilikuwa miongoni mwa wanao fanya maskhara!