(67) Yeye ndiye aliye kuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii, kisha kwa pande la damu, kisha akakutoeni katika hali ya mtoto mchanga, kisha mpate kufikilia utu uzima, kisha mpate kuwa wazee. Na kati yenu wapo wanao kufa kabla, na ili mfikie muda ulio kwisha wekwa, na ili mpate kufahamu.
(68) Yeye ndiye anaye huisha na anaye fisha. Akihukumu jambo liwe, basi huliambia: Kuwa! Likawa.
(69) Je! Huwaoni wale wanao bishana katika Ishara za Mwenyezi Mungu? Wanageuziwa wapi?
(70) Ambao wamekanusha Kitabu na yale tuliyo watuma Mitume wetu. Basi watakuja jua.
(71) Zitakapo kuwa pingu shingoni mwao na minyororo, huku wanabururwa
(72) Katika maji ya moto, kisha wanaunguzwa Motoni,
(73) Tena wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwashirikisha
(74) Badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Wametupotea, bali tangu zamani hatukuwa tukiomba kitu! Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anawaachia makafiri wapotelee mbali.
(75) Haya ni kwa sababu mlikuwa mkijitapa katika ardhi pasipo haki, na kwa sababu mlikuwa mkijishaua.
(76) Ingieni kwenye milango ya Jahannamu, mdumu humo milele. Basi ni maovu yaliyoje makaazi ya wanao takabari!
(77) Basi subiri, hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Na ama tukikuonyesha baadhi ya yale tuliyo waahidi au tukikufisha, lakini wao watarudishwa kwetu tu.