(14) Waambie walio amini wawasamehe wale wasio zitaraji siku za Mwenyezi Mungu, ili awalipe kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
(15) Mwenye kutenda mema basi ni kwa ajili ya nafsi yake, na mwenye kutenda uovu ni juu yake mwenyewe. Kisha mtarudishwa kwa Mola wenu Mlezi.
(16) Na hakika tuliwapa Wana wa Israili Kitabu na hukumu na Unabii, na tukawaruzuku vitu vizuri vizuri, na tukawafadhilisha kuliko walimwengu wote.
(17) Na tukawapa maelezo wazi ya amri. Basi hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa ajili ya uhasidi uliyo kuwa baina yao. Hakika Mola wako Mlezi atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika mambo waliyo kuwa wakikhitalifiana.
(18) Kisha tukakuweka wewe juu ya Njia ya haya mambo, basi ifuate, wala usifuate matamanio ya wasio jua kitu.
(19) Kwa hakika hao hawatakufaa kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hakika wenye kudhulumu ni marafiki wao kwa wao. Na Mwenyezi Mungu ni rafiki wa wamchao.
(20) Hizi ni dalili zilizo wazi kwa watu wote, na ni uwongofu, na rehema kwa watu wanao yakinisha.
(21) Je! Wanadhani wanao tenda maovu kuwa tutawafanya kama walio amini, na wakatenda mema, sawa sawa uhai wao na kufa kwao? Ni hukumu mbaya wanayo ihukumu!
(22) Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki, na ili kila nafsi ilipwe yale iliyo yachuma. Nao hawatadhulumiwa.