(15) Na tumemuusia mwanaadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu. Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini. Hata anapo fika utu uzima wake, na akafikilia miaka arubaini, husema: Mola wangu Mlezi! Niwezeshe nishukuru neema zako ulizo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nitende mema unayo yapenda. Na unitengenezee dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu kwako, na mimi ni miongoni mwa Waislamu.
(16) Hao ndio tunao wapokelea bora ya vitendo vyao walivyo vitenda, na tunayasamehe makosa yao. Watakuwa miongoni mwa watu wa Peponi. Miadi ya kweli hiyo walio ahidiwa.
(17) Na ambaye amewafyonya wazazi wake na akawaambia: Ati ndio mnanitisha kuwa nitafufuliwa, na hali vizazi vingi vimekwisha pita kabla yangu! Na hao wazazi humwomba msaada Mwenyezi Mungu (na humwambia mtoto wao): Ole wako! Amini! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli. Na yeye husema: Hayakuwa haya ila ni visa vya watu wa kale.
(18) Hao ndio ambao imehakikikishwa hukumu juu yao kama mataifa yaliyo kwisha pita kabla yao miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa wenye kukhasiri.
(19) Na wote watakuwa na daraja zao mbali mbali kwa waliyo yatenda, na ili awalipe kwa vitendo vyao, na wala hawatadhulumiwa.
(20) Na siku watakapo letwa walio kufuru kwenye Moto wataambiwa: Nyinyi mlitwaa vitu vyenu vizuri katika uhai wa duniani, na mkastareheshwa navyo. Basi leo ndio mnalipwa adhabu ya fedheha kwa mlivyo kuwa mkitakabari katika ardhi bila ya haki, na kwa sababu mlikuwa mkifanya upotovu.