(12) Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na wakatenda mema katika Bustani zipitiwazo na mito kati yake. Na walio kufuru hujifurahisha na hula kama walavyo wanyama, na Moto ndio makaazi yao.
(13) Na miji mingapi iliyo kuwa na nguvu zaidi kuliko mji wako huu ulio kutoa; nao tuliwateketeza na wala hawakuwa wa kuwanusuru.
(14) Je! Mwenye kuwa na bayana kutoka kwa Mola wake Mlezi ni kama aliye pambiwa uovu wa vitendo vyake, na wakafuata pumbao lao?
(15) Mfano wa Pepo walio ahidiwa wachamngu ina mito ya maji yasiyo vunda, na mito ya maziwa isiyo haribika ladha yake, na mito ya mvinyo yenye ladha kwa wanywao, na mito ya asali iliyo safishwa. Na wao humo watakuwa na kila namna ya matunda, na maghfira kutoka kwa Mola wao Mlezi. Basi hao ni kama watakao dumu Motoni na wakinyweshwa maji yanayo chemka ya kuwakata matumbo yao?
(16) Na wapo miongoni mwao wanao kusikiliza, mpaka wakiondoka kwako huwauliza walio pewa ilimu: Amesema nini sasa hivi? Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao, na wakafuata pumbao lao.
(17) Na wale walio ongoka anawazidishia uongofu na anawapa uchamngu wao.
(18) Kwani wanangojea jengine isipo kuwa iwafikie Saa (ya Kiyama) kwa ghafla? Na hakika alama zake zimekwisha kuja. Na itapo wajia kutawafaa wapi kukumbuka hapo?
(19) Basi jua ya kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, na omba maghufira kwa dhambi zako na za Waumini wanaume na Waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu anajua mahali penu pa kwenda na kurudi, na mahali penu pa kukaa.