(16) Waambie walio achwa nyuma katika mabedui: Mtakuja itwa kwenda pigana na watu wakali kwa vita, mpigane nao au wasalimu amri. Basi mkimt'ii, Mwenyezi Mungu atakupeni ujira mzuri. Na mkigeuka kama mlivyo geuka kwanza, atakuadhibuni kwa adhabu iliyo chungu.
(17) Kipofu hana lawama, wala kiguru hana lawama, wala mgonjwa hana lawama. Na mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, atamuingiza katika Mabustani yapitayo mito kati yake. Na atakaye geuka upande atamuadhibu kwa adhabu chungu.
(18) Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewapa radhi Waumini walipo fungamana nawe chini ya mti, na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao, na akawalipa kwa Ushindi wa karibu.
(19) Na ngawira nyingi watakazo zichukua. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
(20) Mwenyezi Mungu anakuahidini ngawira nyingi mtakazo zichukua, basi amekutangulizieni hizi kwanza, na akaizuia mikono ya watu isikufikieni, na ili hayo yawe ni Ishara kwa Waumini, na akakuongozeni Njia Iliyo Nyooka.
(21) Na mengine hamwezi kuyapata bado, Mwenyezi Mungu amekwisha yazingia. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
(22) Na lau makafiri wangeli pigana nanyi basi bila ya shaka wangeli geuza migongo, kisha wasingeli pata mlinzi wala msaidizi.
(23) Huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu ulio kwisha pita zamani, wala hutapata mabadiliko katika mwendo wa Mwenyezi Mungu.