(12) Enyi mlio amini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anaye penda kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.
(13) Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.
(14) Mabedui wamesema: Tumeamini. Sema: Hamjaamini, lakini semeni: Tumesilimu. Kwani Imani haijaingia katika nyoyo zenu. Na mkimt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hatakupunguzieni chochote katika vitendo vyenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(15) Hakika Waumini ni wale walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake tena wasitie shaka kabisa, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Hao ndio wakweli.
(16) Sema: Ati ndio mnamfundisha Mwenyezi Mungu Dini yenu, na hali Mwenyezi Mungu anayajua ya katika mbingu na ardhi, na Mwenyezi Mungu anajua kila kitu?
(17) Wanakusimbulia kuwa wamesilimu! Sema: Msinisimbulie kwa kusilimu kwenu. Bali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kufanyieni hisani kwa kukuongoeni kwenye Imani, ikiwa nyinyi ni wakweli.
(18) Hakika Mwenyezi Mungu anajua siri za mbingu na ardhi. Na Mwenyezi Mungu anayaona myatendayo.