(10) Na walio kufuru na wakakadhibisha Ishara zetu, hao ni watu wa Motoni, watadumu humo milele. Na hayo ndiyo marudio mabaya.
(11) Haufiki msiba wowote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu huuongoa moyo wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
(12) Na mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume. Mkigeuka, basi hakika juu ya Mtume wetu ni kufikisha (Ujumbe wake) kwa uwazi tu.
(13) Mwenyezi Mungu, hapana mungu isipo kuwa Yeye. Na juu ya Mwenyezi Mungu nawategemee Waumini.
(14) Enyi mlio amini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu wamo maadui zenu. Basi tahadharini nao. Na mkisamehe, na mkapuuza, na mkaghufiria basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu.
(15) Hakika mali yenu na watoto wenu ni jaribio. Na kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa.
(16) Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo, na sikieni, na t'iini, na toeni, itakuwa kheri kwa nafsi zenu. Na mwenye kuepushwa na uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio walio fanikiwa.
(17) Mkimkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, atakuzidishieni mardufu, na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa shukra, Mpole.
(18) Mwenye kujua siri na dhaahiri, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.