(6) Wawekeni humo humo mnamo kaa nyinyi kwa kadiri ya pato lenu, wala msiwaletee madhara kwa kuwadhiki. Na wakiwa wana mimba, wagharimieni mpaka wajifungue. Na wakikunyonyesheeni, basi wapeni ujira wao, na shaurianeni kwa wema. Na mkiona uzito kati yenu, basi amnyonyeshee mwanamke mwengine.
(7) Mwenye wasaa atoe kadiri ya wasaa wake, na mwenye dhiki atoe katika alicho mpa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu ila kwa kadiri ya alicho mpa. Mwenyezi Mungu atajaalia baada ya dhiki faraji.
(8) Na miji mingapi iliyo vunja amri ya Mola wake Mlezi na Mitume wake, basi tuliihisabia hisabu ngumu na tukaiadhibu kwa adhabu kali.
(9) Basi ikauonja ubaya wa mambo yake; na mwisho wa mambo yao ilikuwa khasara.
(10) Mwenyezi Mungu aliwaandalia adhabu kali. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, enyi wenye akili, mlio amini! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteremshieni Ukumbusho,
(11) Mtume anaye kusomeeni Aya za Mwenyezi Mungu zinazo bainisha, ili kuwatoa walio amini na wakatenda mema kutoka gizani kuwapeleka kwenye nuru. Na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, na akatenda mema, atamwingiza katika Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Mwenyezi Mungu amekwisha mpa riziki nzuri.
(12) Mwenyezi Mungu ni yule ambaye ameziumba mbingu saba, na ardhi kwa mfano wa hizo. Amri zake zinashuka baina yao, ili mjue kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu, na kwamba Mwenyezi Mungu amekizunguka kila kitu kukijua vilivyo kwa ilimu yake.