(41) NA JUENI ya kwamba ngawira mnayo ipata, basi khums (sehemu moja katika tano) ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume, na jamaa, na mayatima, na masikini, na wasafiri, ikiwa nyinyi mmemuamini Mwenyezi Mungu na tuliyo yateremsha kwa mja wetu siku ya kipambanuo, siku yalipo kutana majeshi mawili. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
(42) Kumbukeni pale mlipo kuwa nyinyi kwenye ng'ambo ya karibu ya bonde, na wao wakawa ng'ambo ya mbali, na msafara ulipo kuwa chini yenu. Na ingeli kuwa mmeagana mngeli khitalifiana katika miadi. Lakini (mkakutana) ili Mwenyezi Mungu atimize jambo lilio kuwa lazima litendeke, kwa sababu aangamie wa kuangamia kwa dalili zilizo dhaahiri, na asalimike wa kusalimika kwa dalili zilizo dhaahiri. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
(43) Kumbuka alipo kuonyesha usingizini mwako kwamba wao ni wachache - na lau angeli kuonyesha kuwa ni wengi, mngeli ingiwa na woga, na mngeli zozana katika jambo hilo. Lakini Mwenyezi Mungu kakuvueni. Hakika Yeye ni Mwenye kuyajua yalio vifuani.
(44) Na mlipo kutana akakuonyesheni machoni mwenu kuwa wao ni wachache, na akakufanyeni nyinyi ni wachache machoni mwao, ili Mwenyezi Mungu atimize jambo lilio kuwa liwe. Na mambo yote hurejezwa kwa Mwenyezi Mungu.
(45) Enyi mlio amini! Mkikutana na jeshi, basi kueni imara, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu sana ili mpate kufanikiwa.