التين At-Tin
(1) Naapa kwa tini na zaituni!
(2) Na kwa Mlima wa Sinai!
(3) Na kwa mji huu wenye amani!
(4) Bila ya shaka tumemuumba mtu kwa umbo lilio bora kabisa.
(5) Kisha tukamrudisha kuwa chini kuliko walio chini!
(6) Lakini wale walio amini na wakatenda mema, hao watapata ujira usio kwisha.
(7) Basi ni kipi baadaye kitacho kukukadhibishia malipo?
(8) Kwani Mwenyezi Mungu si muadilifu kuliko mahakimu wote?
العلق Al-Alaq
(1) Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba,
(2) Amemuumba binaadamu kwa tone la damu,
(3) Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote!
(4) Ambaye amefundisha kwa kalamu.
(5) Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui.
(6) Kwani! Hakika mtu bila ya shaka huwa jeuri
(7) Akijiona katajirika.
(8) Hakika kwa Mola wako Mlezi ndio marejeo.
(9) Umemwona yule anaye mkataza
(10) Mja anapo sali?
(11) Umeona kama yeye yuko juu ya uwongofu?
(12) Au anaamrisha uchamngu?
(13) Umeona kama yeye akikanusha na anarudi nyuma?
(14) Hajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anaona?
(15) Kwani! Kama haachi, tutamkokota kwa shungi la nywele!
(16) Shungi la uwongo, lenye makosa!
(17) Basi na awaite wenzake!
(18) Nasi tutawaita Mazabania!
(19) Hasha! Usimt'ii! Nawe sujudu na ujongee!