(70) Na alipo kwisha watengenezea mahitaji yao akakitia kikopo cha kunywea maji katika mzigo wa nduguye huyo, kisha mnadi akanadi: Enyi wasafiri! Hapana shaka nyinyi ni wezi!
(71) Wakasema nao wamewakabili: Kwani mmepoteza nini?
(72) Wakasema: Tumepoteza kopo la mfalme. Na ataye lileta atapewa shehena nzima ya ngamia. Nami ni dhaamini wa hayo.
(73) Wakasema: Wallahi! Mnajua vyema kwamba sisi hatukuja kufanya uharibifu katika nchi hii, wala sisi si wezi.
(74) Wakasema: Basi malipo yake yatakuwa nini ikiwa nyinyi ni waongo?
(75) Wakasema: Malipo yake ni yule ambaye ataonekana nalo yeye huyo ndiye malipo yake. Hivi ndivyo tunavyo walipa madhaalimu.
(76) Basi akaanza kwenye mizigo yao kabla ya mzigo wa nduguye. Kisha akakitoa katika mzigo wa nduguye. Hivi ndivyo tulivyo mpangia Yusuf. Hakuweza kumzuia nduguye kwa sharia ya mfalme isipo kuwa alivyo taka Mwenyezi Mungu. Tunawatukuza kwenye vyeo tuwatakao; na juu ya kila ajuaye yupo ajuaye zaidi.
(77) Wakasema: Ikiwa huyu ameiba, basi nduguye vile vile aliiba zamani. Lakini Yusuf aliyaweka siri moyoni mwake wala hakuwaonyesha. Akawaambia: Nyinyi mko katika hali mbaya zaidi, na Mwenyezi Mungu anajua zaidi hayo mnayo singizia.
(78) Wakasema: Ewe Mheshimiwa! Huyu anaye baba mzee sana. Kwa hivyo mchukue mmoja wetu badala yake. Hakika sisi tunakuona wewe ni katika watu wema.