(118) Na Mola wako Mlezi angeli penda ange wafanya watu wote wakawa umma mmoja. Lakini hawaachi kukhitalifiana,
(119) Isipo kuwa wale ambao Mola wako Mlezi amewarehemu; na kwa hiyo ndio Mwenyezi Mungu amewaumba. Na litatimia neno la Mola wako Mlezi: Kweli kweli nitaijaza Jahannam kwa majini na watu pamoja.
(120) Na yote tunayo kusimulia katika khabari za Mitume ni ya kukupa nguvu moyo wako. Na katika haya imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa Waumini.
(121) Na waambie wale wasio amini: Fanyeni muwezavyo, nasi pia tunafanya.
(122) Na ngojeni, na sisi tunangoja.
(123) Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyo fichikana katika ardhi na mbingu, na mambo yote yatarejezwa kwake. Basi muabudu Yeye na umtegemee Yeye. Na Mola wako Mlezi haghafiliki na yale mnayo yatenda.
يوسف Yusuf
(1) Alif Lam Raa. Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha.
(2) Hakika Sisi tumeiteremsha Qur'ani kwa Kiarabu ili mpate kuzingatia.
(3) Sisi tunasimulia simulizi nzuri kwa kukufunulia Qur'ani hii. Na ijapo kuwa kabla ya haya ulikuwa miongoni mwa wasio jua.
(4) Yusuf alipo mwambia baba yake: Ewe babaangu! Hakika mimi nimeota nyota kumi na moja, na jua, na mwezi. Nimeota zikinisujudia.