(14) Wa kuombwa kweli ni Yeye tu. Na hao wanao waomba badala yake hawawajibu chochote; bali ni kama mwenye kunyoosha viganja vyake kwenye maji ili yafike kinywani mwake, lakini hayafiki. Na maombi ya makafiri hayako ila katika upotovu.
(15) Na viliomo mbinguni na katika ardhi vinamsujudia Mwenyezi Mungu tu vikitaka visitake. Na pia vivuli vyao asubuhi na jioni.
(16) Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu na ardhi? Sema: Mwenyezi Mungu. Sema: Basi je, mnawafanya wenginewe badala yake kuwa ni walinzi, nao hawajifai wenyewe kwa jema wala baya? Sema: Hebu kipofu na mwenye kuona huwa sawa? Au hebu huwa sawa giza na mwangaza? Au wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika walio umba kama alivyo umba Yeye, na viumbe hivyo vikawadanganyikia? Sema: Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu. Na Yeye ni Mmoja Mwenye kushinda!
(17) Ameteremsha maji kutoka mbinguni. Na mabonde yakamiminika maji kwa kadiri yake. Na mafuriko yakachukua mapovu yaliyo kusanyika juu yake. Na kutokana na wanavyo yayusha katika moto kwa kutaka mapambo au vyombo hutokea povu vile vile. Namna hivyo Mwenyezi Mungu ndivyo anavyo piga mifano ya Haki na baat'ili. Basi lile povu linapita kama takataka tu basi. Ama kinacho wafaa watu hubakia kwenye ardhi. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo piga mifano.
(18) Walio muitikia Mola wao Mlezi watapata wema. Na wasio muitikia, hata wangeli kuwa navyo vyote viliomo katika ardhi na mfano wa hivyo, bila ya shaka wangeli vitoa kujikombolea! Hao watapata hisabu mbaya kabisa, na makao yao ni Jahannamu. Na hapo ni pahala pabaya mno!